Ziko tofauti nyingi za kijinsia kati ya wanawake na
wanaume, ambazo mara nyingi zimekuwa chanzo cha migongano, migogoro na mivutano
katika ndoa. Kutokuzifahamu tofauti hizi kumesababisha wanandoa kupeana upendo
ambao kila mmoja angependa apatiwe, badala ya upendo ambao mwenzake angependa
apatiwe yeye, kulingana na silika ya jinsia yake.
Mara nyingi wanawake wamewapa wanaume malezi ya kuwajali, badala ya malezi ya kuonyesha
kuwa na Imani nao. Wakati huo huo,
wanaume wamewapa wanawake malezi kuonyesha kuwa
na Imani nao, badala ya malezi ya kuwajali.
Kutokana na mpishano huu, ndoa nyingi zimejikuta katika mivutano mingi, na
changamoto ya kutokuridhishana, kwa pande zote mbili.
Utakuta, kwa vile mahitaji ya mwanamke ya msingi ya
hisia za moyo ni mwenzi wake kumjali,
basi anafikiri ndiyo mahitaji ya msingi ya mwanaume pia. Vivyo hivyo, utakuta
mwanaume anataka mpenzi wake aonyeshe kuwa na imani naye. Hivyo, anajaribu kutoa mapenzi ya kuonyesha kuwa na Imani
kwa mwenzi wake hitaji ambalo yeye angependa apatiwe na huyo mwenzi wake. Kila
mmoja, pasipo kujua, anatoa aina ya mapenzi ambayo yeye angependa apatiwe,
badala ya mapenzi ambayo mwenzi wake angependa apatiwe, kutokana na tofauti ya
kijinsia aliyonayo.
Kwa kuelewa tofauti hizi za jinsia, na kwa kujitahidi
kuuweka ufahamu huo katika matendo, misuguano iliyoko katika ndoa kati ya
wanawake na wanaume itaweza kupungua kwa kiasi kikubwa. Ingawa hii pekee yake
haitoshi kumaliza mivutano na migogoro katika ndoa, lakini ni moja ya njia
muhimu ya kuboresha mahusiano katika ndoa.
Kuna wanandoa ambao, hata pasipo ufahamu huu, wameweza
kuchukualiana na kuishi pamoja kwa mafanikio, na kuweza kuoanisha tofauti hizi
za kijinsia. Hii ni kutokana na kipawa na alichonacho mmojawapo au wote wawili,
katika kuoanisha tofauti hizi. Lakini, kufanikiwa huku pasipokuwa na ufahamu
huu kunatokana na kipawa cha kuzaliwa.
Lakini hata kama mtu anacho kipawa cha kuzaliwa,
kukiboresha kupitia kuongeza ufahamu ni jambo la msingi. Hata kama ndoa ni
bora, siku zote kuna nafasi ya kuzidi kuboresha zaidi na zaidi kupitia kuongeza
ufahamu kuhusu ndoa. Maarifa siku zote ni silaha. Yaani maarifa yanampa mtu
uwezo wa kutawala jambo.
Dr. Abraham Maslow, mwanasaikolojis mashuhuri wa karne
ya ishirini, anaeleza kuhusu ufahamu na maarifa, kama ifuatavyo;
Elimu,
ujuzi, ufahamu, kuijua kweli, na udhihirisho ni tiba ya hali ya juu…….na kama ufahamu unatibu, basi kukosa ufahamu
kunasababisha kuugua.
Maarifa, ufahamu, ujuzi au elimu ni silaha muhimu sana
kwa binadamu, silaha ambayo ikimpa kudhibiti mambo, na kutawala changamoto
mbalimbali katika maisha yake. Na katika ndoa pia, maarifa yanayohusu ndoa ni moja ya mhimili muhimu.
Ili kupata makala hizi kwenye barua pepe yako jaza kisanduku hicho pembeni mkono wa kulia.
Ili kupata makala hizi kwenye barua pepe yako jaza kisanduku hicho pembeni mkono wa kulia.
No comments:
Post a Comment