Tuesday 4 April 2017

JIFUNZE MAARIFA YA KUIFANYA NDOA YAKO KUWA NA FURAHA DAIMA

Leo ningenda turudie mada ambayo tulikwishaiongelea hapa awali kuhusu tofauti za kijinsia ambazo nyingi kati ya hizo zimekuwa ni kiini cha migogoro ya hapa na pale katika maisha yetu ya ndoa.

Ziko tofauti nyingi za kijinsia kati ya wanawake na wanaume, ambazo mara nyingi zimekuwa chanzo cha migongano, migogoro na mivutano katika ndoa. Kutokuzifahamu tofauti hizi kumesababisha wanandoa kupeana upendo ambao kila mmoja angependa apatiwe, badala ya upendo ambao mwenzake angependa apatiwe yeye, kulingana na silika ya jinsia yake. 

Mara nyingi wanawake wamewapa wanaume malezi ya kuwajali, badala ya malezi ya kuonyesha kuwa na Imani nao. Wakati huo huo, wanaume wamewapa wanawake malezi kuonyesha kuwa na Imani nao, badala ya malezi ya kuwajali. Kutokana na mpishano huu, ndoa nyingi zimejikuta katika mivutano mingi, na changamoto ya kutokuridhishana, kwa pande zote mbili.

Utakuta, kwa vile mahitaji ya mwanamke ya msingi ya hisia za moyo ni mwenzi wake kumjali, basi anafikiri ndiyo mahitaji ya msingi ya mwanaume pia. Vivyo hivyo, utakuta mwanaume anataka mpenzi wake aonyeshe kuwa na imani naye. Hivyo, anajaribu kutoa mapenzi ya kuonyesha kuwa na Imani kwa mwenzi wake hitaji ambalo yeye angependa apatiwe na huyo mwenzi wake. Kila mmoja, pasipo kujua, anatoa aina ya mapenzi ambayo yeye angependa apatiwe, badala ya mapenzi ambayo mwenzi wake angependa apatiwe, kutokana na tofauti ya kijinsia aliyonayo.

Kwa kuelewa tofauti hizi za jinsia, na kwa kujitahidi kuuweka ufahamu huo katika matendo, misuguano iliyoko katika ndoa kati ya wanawake na wanaume itaweza kupungua kwa kiasi kikubwa. Ingawa hii pekee yake haitoshi kumaliza mivutano na migogoro katika ndoa, lakini ni moja ya njia muhimu ya kuboresha mahusiano katika ndoa.

Kuna wanandoa ambao, hata pasipo ufahamu huu, wameweza kuchukualiana na kuishi pamoja kwa mafanikio, na kuweza kuoanisha tofauti hizi za kijinsia. Hii ni kutokana na kipawa na alichonacho mmojawapo au wote wawili, katika kuoanisha tofauti hizi. Lakini, kufanikiwa huku pasipokuwa na ufahamu huu kunatokana  na kipawa cha kuzaliwa.

Lakini hata kama mtu anacho kipawa cha kuzaliwa, kukiboresha kupitia kuongeza ufahamu ni jambo la msingi. Hata kama ndoa ni bora, siku zote kuna nafasi ya kuzidi kuboresha zaidi na zaidi kupitia kuongeza ufahamu kuhusu ndoa. Maarifa siku zote ni silaha. Yaani maarifa yanampa mtu uwezo wa kutawala jambo.

Dr. Abraham Maslow, mwanasaikolojia mashuhuri wa karne ya ishirini, anaeleza kuhusu ufahamu na maarifa, kama ifuatavyo;
Elimu, ujuzi, ufahamu, kuijua kweli, na udhihirisho ni tiba ya hali ya juu…….na kama     ufahamu unatibu, basi kukosa ufahamu kunasababisha kuugua.

Maarifa, ufahamu, ujuzi au elimu ni silaha muhimu sana kwa binadamu, silaha ambayo ikimpa kudhibiti mambo, na kutawala changamoto mbalimbali katika maisha yake. Na katika ndoa pia, maarifa yanayohusu ndoa ni moja ya mhimili muhimu.


No comments:

Post a Comment