Saturday, 14 May 2016

NJAA MBILI (2) ZINAZOWASUMBUA WANADOA KATIKA MAISHA YAO YA NDOA


Habari rafiki na mpenzi msomaji wa wavuti hii. Na karibu tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza. Katika makala yetu ya leo tutajifunza njaa zinazowasumbua wanandoa katika maisha yao ya ndoa. Kuzifahamu njaa zinazowasumbua wanandoa tafadhali twende sanjari mpaka mwisho wa makala hii.

Kumekuwa na mitazamo hasi sana juu ya maisha ya ndoa. Kabla mtu hajaingia ndani ya maisha ya ndoa tayari akili yake imeshajazwa mitazamo hasi juu ya maisha ya ndoa. Mtu aliyepatwa na matatizo katika maisha yake ya ndoa naye atakwenda kuwaaminisha watu juu ya matatizo yake juu ya ndoa. Siyo kwamba katika maisha ya ndoa hakuna changamoto la hasha zipo kama kawaida kama vile kwenye kazi, biashara, ujasiriamali nakadhalika. Hivyo kwenye jambo lolote changamoto haziepukiki. Kweli itakuweka huru na usipoujua ukweli utapata shida sana. Maisha ya ndoa unayotaka kuishi unayatengeneza wewe mwenyewe na si vinginevyo hivyo usipoteze muda wa kuhangaika tengeneza yale maisha ambayo unayataka kuishi na usisikilize kelele za watu ambazo zitakuwekea ukungu katika macho yako na kushindwa kuona mbele. Na waswahili wanasema ukiona vyaelea ujue vimeundwa kwa hiyo, hata wewe unaweza kuviunda katika maisha yako ya ndoa.

Katika hali ya kawaida hakuna mtu asiyeijua njaa, mtu akiwa na njaa anapoteza kabisa nguvu na hata ufanisi wa kazi aliyokuwa anafanya unapotea, kwa hiyo njaa huwa inalegeza watu kama akikosa kula chakula na kushiba. Vivyo hivyo, kila mwanandoa ana njaa yake yaani mwanaume ana njaa yake katika maisha ya ndoa hali kadhalika kwa mwanamke naye ana njaa yake. Kwa maana hiyo, kila mwanandoa anahitaji ashibishwe njaa yake na mwenza wake. Ikitokea sasa wanandoa hao yaani wawili hao kutoshibishana njaa zao ndio matatizo huanzia hapo. Na tunajua ya kwamba wawili hao kila mmoja ana njaa yake. Hivi ikitokea mtu ana njaa ya chakula halafu pale anapotegemea kupata chakula ili ashibishe njaa yake hapati ataendelea kusubiri kubaki na njaa yake? Jibu ni kwamba lazima atatafuta sehemu ambayo ataweza kupata chakula ili aweze kushibisha njaa yake.
Ndugu msomaji, kama kila mwanandoa ameshindwa kumshibisha mwenzake basi ujue lazima atatafuta chakula sehemu nyingine ili kuweza kukidhi njaa yake. Hivyo basi, kumbe ni wajibu wa kila mwanandoa kuhakikisha anamshibisha mwenzake njaa yake.

Zifuatazo ni njaa mbili zinazowasumbua wanandoa endapo hawatashibishana;


1. Njaa ya mwanamke ni upendo;


Mwanamke anahitaji upendo kuliko vitu vingine, hata katika vitabu vya dini vinasema; enyi waume, wapendeni wake zenu. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe, mwanaume anatakiwa kujitoa kwelikweli kumpenda mke wake kama tunavyojua upendo ndio falsafa kubwa sana katika maisha ya binadamu, upendo huvumilia, hufadhili, hauhusudu. Hivyo basi njaa ya mwanamke ni kupendwa. Wewe kama mwanaume unatakiwa kumpenda mke wako kwa moyo wako wote bila kujali udhaifu wake. Hii ndio njaa ya wanawake wanahitaji upendo katika maisha ya ndoa.

2. Njaa ya mwanaume ni kuheshimiwa;


Mwanaume njaa yake kubwa ni kuheshimiwa katika maisha ya ndoa. Sasa ikitokea mwanaume anakosa kuheshimiwa na mke wake katika maisha ya ndoa hivyo anakuwa amekosa kushibishwa njaa yake. Na kama akikosa kushiba ndio matatizo huanzia hapo itamlazimu kutafuta kushibishwa njaa yake nje. Hivyo kama wewe ni mwanamke unatakiwa kumshibisha mume wako njaa yake ya kumtii.

Kama wanandoa wanashindwa kushibishana njaa zao, hivyo wanajitengenezea shimo wao wenyewe. Watu wanajisahau sana katika kutimiza majukumu yao katika maisha ya ndoa hatimaye wanaruhusu haki za kibinadamu kuingia maisha ya ndoa, kama wanandoa mkishaingiza haki za kibinadamu katika maisha ya ndoa yaani hamsini kwa hamsini kama wanavyodai lazima mtapoteza mwelekeo tu. Kwa hiyo kila mtu ana njaa yake kama tulivyoona hapo juu sasa mkishayaingiza mambo haya ya kidunia mtakosa kushibishana njaa zenu.

Mwisho, kila mwanandoa ana wajibu wa kumshibisha mwenza wake, mke akipendwa atashiba njaa yake na mume akiheshimiwa atashiba njaa yake. Kila mtu ana njaa yake hivyo mnatakiwa kushibishana na kupendana katika shida na raha.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

Tuesday, 10 May 2016

JINSI UNAVYOWEZA KUMJENGEA MTAZAMO CHANYA MTOTO WAKO


Kuna msemo ‘usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’. Ni msemo ambao mara kwa mara huwafundisha wazazi umuhimu wa kulea watoto wao katika maadili mema na ya kimafanikio. Mara nyingi ikumbukwe kwamba wazazi huwa ndio wenye jukumu kubwa sana la kulea watoto wao tofauti na watu wengine kama walimu, madaktari na jamii, jukumu la kwanza huwa lipo kwa mzazi.

Hapa mzazi huwa ana kazi kubwa sana kumbuka tu si tu ya kumlea huyu mtoto katika mazingira hatarishi peke yake yatakayomdhuru, lahasha bali huwa ana jukumu pia la kuhakikisha mtoto huyu anakulia katika malezi bora ambayo yatampelekea awe na mtazamo chanya katika maisha yake siku zote.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya walezi ya watoto wanadai kwamba msingi mkubwa wa maisha ya binadamu huwa unajengwa kuanzia miaka 0-12. Hiyo ikiwa na maana kama mtoto wako utamlea vizuri kwenye umri huu basi elewa atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa tofauti na yule ambaye atalelewa katika maadili mabovu.

Mpaka hapo unaweza ukawa umeona kwamba umri wa kuwa makini na mtoto wako ni umri huu ambao upo chini ya miaka 12. Katika umri huu, hapa wengi ndipo wanapoharibu au kutengeneza watoto wao. Kama unafikiri natania jaribu kufatilia wale watoto ambao wamevuka umri huu. Kwa tabia yoyote atakayokuwa nayo msingi wake mkubwa umetokea kwenye miaka 0-12.

Kwa kulifafanua hili vizuri, nikiwa na maana kama mtoto wako unaona ana tabia mbaya basi elewa kabisa ulimharibu tokea akiwa chini ya miaka 12 na wala usisingizie kitu chochote nje ya hapo. Na ndiyo maana ni hatari sana kwa mzazi kumpeleka mtoto wake chini ya umri huu shule za boarding kwa sababu huu ndiyo umri ambao mtoto anatakiwa apewe msingi bora wa maisha ikishindikana hapo basi tena.

Kwa hiyo kitu cha msingi katika umri ni kumpa mtoto malezi bora yatakamfanya ajitambue zaidi. Malezi haya kwa bahati mbaya tofauti na wengi wanavyofikiri hawezi kupewa na mwalimu au na mtu mwingine yoyote kwa ubora wa hali ya juu zaidi ya mzazi. Kwani ni kipindi ambacho unatakiwa umfundishe mtoto wako juu ya mambo mengi kama upendo, kujali, utunzaji mzuri wa fedha, utu, kuokoa muda, kutoa, kujiamini na mambo mengineyo mengi.

Kwa kukosa mambo hayo baadae hupelekea mtoto huyu kuanza kuteseka kujifunza upya na tena kwa tabu lakini kumbe wakati alitakiwa kujifunza akiwa mdogo tena kwa urahisi . kwa kulijua hili leo unaweza ukaanza na kumfundisha mtoto wako namna ya kumjengea mtazamo chanya ambao utamfanya ajiamini na kufanya vizuri katika kila eneo la maisha kwa ubora wa hali ya juu.

Je, unawezaje kumjengea moto wako mtazamo chanya?

1. Msifie.

Jijengee tabia ya kumsifia mtoto wako kwa yale mambo madogo anayoyafanya. Acha kumkosoa na kiasi cha kwamba kujiona hafai. Hakikisha unampa sifa. Sifa hizo itakuwa nzuri sana kama utakuwa unampa hadharani mbele ya wenzake. Hilo litamfanya ajiamini zaidi na kujiona yeye anaweza. Kwa kadri utakavyoendelea kumsifia atajikuta mtoto wako anazidi kuwa mwenye uwezo mzuri wa kujiamini sana.

 

 
MSIFIE MTOTO WAKO ANAPOFANYA JAMBO ZURI
 


2. Mwamini.

Mbali na kumpa sifa, lakini pia unaweza kumjengea mtoto wako tabia nzuri ya kujiamini kwa wewe kumwamini pia katika yale mambo anayofanya. Kama ni kazi umemwachia, mwache aifanye akiwa peke yake huku ukiwa unamfatilia sio sana ili kuona anafanyaje. Kwa kitendo cha kumfanyia hivyo atajiona kuwa yeye kumbe anaweza kufanya mambo makubwa na hivyo atajikuta akiwa anajiamini.

3. Mpe majina mazuri.

Weka utararibu wa kumpa mtoto wako majina mazuri yatakayomfanya ajiamini. Kila unapokutana naye mbali na kumuita jina lake halisi unaweza ukamuita ‘Pilot, shujaa, mshindi, mtaalamu’ na mengineyo mengi yatakamfanya ajiamini na kujiona bora kuliko. Epuka kumpa ‘lebo’ za kumuita majina kama vile ‘mjinga wewe, kichwa maji we’. Hiyo itamkatisha tamaa na itamfanya ashindwe kujiamini.

4. Mpe mazoezi ya kuongea mbele za wenzake.

Anapokuwa na wenzake tafuta kitu cha kuongea na kumfanya aongee mbele za wenzake. Hata kama anaona aibu mpe moyo wa kumfanya aendelee kuongea. Kwa kitendo hicho kitamfanya azidi kujiamini sana na itampelekea kweli kuongeza uwezo wake mkubwa wa kujiamini siku hadi siku. Hata wakati mwingine hata kuwa na ule woga mkubwa ndani yake wa kuzungumza.

Unaweza ukafanya mambo mengi yatakayomfanya mtoto wako azidi kujiamini. Lakini kwa leo fanyia kazi kwanza hayo na hakikisha mtoto wako anaweza kujiamini kwa namna yoyote ile. Hiyo itamsaidia sana kwa maisha yake yote ya baade.

Kwa makala nyingine nzuri pia tembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika kila siku.

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani ngwangwalu,

Simu; 0713 048 035,