Friday 19 May 2017

MAZOEA SABA (7) MABAYA KWA WANANDOA

Napenda tena kuchukua nafasi hii adimu kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na nchi kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha kwenu baadhi ya mazoea mabaya ustawi ndoa ambayo hufanywa na wanandoa wengi. Pia napenda kuwashukuru wale wote waliopata nafasi ya kusoma makala zangu kwa maoni na mawazo yenu mazuri, napenda kuchukua nafasi hii kuwaombeni mwaalike na wenzenu kusoma makala zangu ambazo huwa natoa kila wiki.
Leo nitaongelea makosa saba (7) ambayo mara nyinyi hufanywa na wanandoa na kusababisha kuibuka kwa migogoro katika mahusiano. Makosa hayo ni kama yafuatavyo: -
1.   Kususia tendo la ndoa bila sababu ya msingi; Tendo la ndoa ni mmojawapo wa nguzo muhimu ya ndoa zote. Kwa hiyo, inapotokea mmoja wa wanandoa kuamua kumnyima mwenzake tendo la ndoa bila sababu ya msingi ni tendo ambalo linaweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa bila kujali ni ya kidini, kimila au kiserikali.
2.   Kumsema vibaya mwenzako wako kwa rafiki/ndugu; Ni makosa makubwa sana kwa mustakabali wa ndoa kwa mmoja wa wanandoa kumsema vibaya mwenzake kwa rafiki zake au ndugu zake badala ya kumuelimisha ili kuondoa  kasoro unazoziona kwake.
3.   Kutotimiza yale unayosema; Ni kosa kubwa sana kwa mwanandoa kutotimiza/kutenda yale anayoahidi kwa mkewe/mmewe bila sababu ya msingi. Katika mahusiano hutokea misukosuko ya hapa na pale na nyingi hutokea mmoja wa wanandoa kuomba msamaha na kukiri kutorudia vitendo fulani ambavyo ni kero kwa mwenzako kwa mfano; kulala nje, kuchelewa kurudi nyumbani bila taarifa yo yote, nakadhalika.
4.   Kutokukubali makosa; Ni busara kwa mstakabali mzuri wa ndoa kukubali makosa inapotokea kuwa mmoja wa wanandoa kafanya makosa. Imekuwa ni vigumu sana kwa wanandoa hasa wanaume kukubali makosa inapotokea wamefanya makosa na badala yake huonyesha kukiri kwa vitendo yaani; kufuata mapendekezo ya wake zao na siyo kukubali kwamba maamuzi yao ya awali yalikuwa na makosa. Si dhambi kukiri kufanya maamuzi kimakosa inapotokea kwa mustakabali mwema wa mahusiano.
5.   Kuwa na hasira zisizo na mpangilio; Ni makosa makubwa kuwa na hasira zisizo na mpangilio kwa mwenzako au kuhamisha hasira kutoka ofisini au kwenye shughuli yo yote unayoifanya na kuzipeleka nyumbani.
Nyumbani ni mahali ambapo inakiwa iwe ni pakupatia faraja na pumziko stahili.
6.   Kutojishughulisha na kumuelewa mwenzako; Ni jambo jema kwa mustakabali mzuri mahusiano kufanya jitihadi kumuelewa mwenzako anakuweje katika hali ya furaha au huzuni. Hili ni muhimu sana katika mahusiano hata katika urafiki wa kawaida. Hii ni nguzo muhimu sana katika kudumisha mahusiano kwa wanandoa. Kinyume cha hapo ni kujenga mifarakano isiyo lazoma.
7.   Kutomshukuru mwenzako anapokuwa amefanya jambo zuri; Ni vizuri inapotokea mwanaume/mwanamke kafanya jambo jema kumshukuru ili kumpa moyo wa kufanya vizuri zaidi siku nyingine. Kwa mfano kama mwanaume/mwanamke ameamua kwa upendo kukununulia zaidi ya nguo ni busara kumshukuru kwanza kwa zawadi hiyo badala ya kulaumiwa kwamba nguo hiyo siyo nzuri au imeshapitwa na wakati, umeuziwa bei mbaya, karudishe nakadhalika.
Mambo yote hayo niliyoyataja hapo juu yanaweza kuepukwa, iwapo utakuwa mtafiti  na utamweka Mungu karibu  katika maisha yako yote.  Na pia kwa ushauri naomba tuwasilianae kwa barua pepe ya fkmwamoto@gmail.com  kwa ushauri makini wa masuala ya mahusiano.



Tuesday 4 April 2017

JIFUNZE MAARIFA YA KUIFANYA NDOA YAKO KUWA NA FURAHA DAIMA

Leo ningenda turudie mada ambayo tulikwishaiongelea hapa awali kuhusu tofauti za kijinsia ambazo nyingi kati ya hizo zimekuwa ni kiini cha migogoro ya hapa na pale katika maisha yetu ya ndoa.

Ziko tofauti nyingi za kijinsia kati ya wanawake na wanaume, ambazo mara nyingi zimekuwa chanzo cha migongano, migogoro na mivutano katika ndoa. Kutokuzifahamu tofauti hizi kumesababisha wanandoa kupeana upendo ambao kila mmoja angependa apatiwe, badala ya upendo ambao mwenzake angependa apatiwe yeye, kulingana na silika ya jinsia yake. 

Mara nyingi wanawake wamewapa wanaume malezi ya kuwajali, badala ya malezi ya kuonyesha kuwa na Imani nao. Wakati huo huo, wanaume wamewapa wanawake malezi kuonyesha kuwa na Imani nao, badala ya malezi ya kuwajali. Kutokana na mpishano huu, ndoa nyingi zimejikuta katika mivutano mingi, na changamoto ya kutokuridhishana, kwa pande zote mbili.

Utakuta, kwa vile mahitaji ya mwanamke ya msingi ya hisia za moyo ni mwenzi wake kumjali, basi anafikiri ndiyo mahitaji ya msingi ya mwanaume pia. Vivyo hivyo, utakuta mwanaume anataka mpenzi wake aonyeshe kuwa na imani naye. Hivyo, anajaribu kutoa mapenzi ya kuonyesha kuwa na Imani kwa mwenzi wake hitaji ambalo yeye angependa apatiwe na huyo mwenzi wake. Kila mmoja, pasipo kujua, anatoa aina ya mapenzi ambayo yeye angependa apatiwe, badala ya mapenzi ambayo mwenzi wake angependa apatiwe, kutokana na tofauti ya kijinsia aliyonayo.

Kwa kuelewa tofauti hizi za jinsia, na kwa kujitahidi kuuweka ufahamu huo katika matendo, misuguano iliyoko katika ndoa kati ya wanawake na wanaume itaweza kupungua kwa kiasi kikubwa. Ingawa hii pekee yake haitoshi kumaliza mivutano na migogoro katika ndoa, lakini ni moja ya njia muhimu ya kuboresha mahusiano katika ndoa.

Kuna wanandoa ambao, hata pasipo ufahamu huu, wameweza kuchukualiana na kuishi pamoja kwa mafanikio, na kuweza kuoanisha tofauti hizi za kijinsia. Hii ni kutokana na kipawa na alichonacho mmojawapo au wote wawili, katika kuoanisha tofauti hizi. Lakini, kufanikiwa huku pasipokuwa na ufahamu huu kunatokana  na kipawa cha kuzaliwa.

Lakini hata kama mtu anacho kipawa cha kuzaliwa, kukiboresha kupitia kuongeza ufahamu ni jambo la msingi. Hata kama ndoa ni bora, siku zote kuna nafasi ya kuzidi kuboresha zaidi na zaidi kupitia kuongeza ufahamu kuhusu ndoa. Maarifa siku zote ni silaha. Yaani maarifa yanampa mtu uwezo wa kutawala jambo.

Dr. Abraham Maslow, mwanasaikolojia mashuhuri wa karne ya ishirini, anaeleza kuhusu ufahamu na maarifa, kama ifuatavyo;
Elimu, ujuzi, ufahamu, kuijua kweli, na udhihirisho ni tiba ya hali ya juu…….na kama     ufahamu unatibu, basi kukosa ufahamu kunasababisha kuugua.

Maarifa, ufahamu, ujuzi au elimu ni silaha muhimu sana kwa binadamu, silaha ambayo ikimpa kudhibiti mambo, na kutawala changamoto mbalimbali katika maisha yake. Na katika ndoa pia, maarifa yanayohusu ndoa ni moja ya mhimili muhimu.