Kuna msemo ‘usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’. Ni msemo
ambao mara kwa mara huwafundisha wazazi umuhimu wa kulea watoto wao katika
maadili mema na ya kimafanikio. Mara nyingi ikumbukwe kwamba wazazi huwa ndio
wenye jukumu kubwa sana la kulea watoto wao tofauti na watu wengine kama
walimu, madaktari na jamii, jukumu la kwanza huwa lipo kwa mzazi.
Hapa mzazi huwa ana kazi kubwa sana kumbuka tu si tu ya kumlea
huyu mtoto katika mazingira hatarishi peke yake yatakayomdhuru, lahasha bali
huwa ana jukumu pia la kuhakikisha mtoto huyu anakulia katika malezi bora
ambayo yatampelekea awe na mtazamo chanya katika maisha yake siku zote.
Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya walezi ya watoto wanadai
kwamba msingi mkubwa wa maisha ya binadamu huwa unajengwa kuanzia miaka 0-12.
Hiyo ikiwa na maana kama mtoto wako utamlea vizuri kwenye umri huu basi elewa
atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa tofauti na yule ambaye atalelewa katika
maadili mabovu.
Mpaka hapo unaweza ukawa umeona kwamba umri wa kuwa makini na
mtoto wako ni umri huu ambao upo chini ya miaka 12. Katika umri huu, hapa wengi
ndipo wanapoharibu au kutengeneza watoto wao. Kama unafikiri natania jaribu
kufatilia wale watoto ambao wamevuka umri huu. Kwa tabia yoyote atakayokuwa
nayo msingi wake mkubwa umetokea kwenye miaka 0-12.
Kwa kulifafanua hili vizuri, nikiwa na maana kama mtoto wako
unaona ana tabia mbaya basi elewa kabisa ulimharibu tokea akiwa chini ya miaka
12 na wala usisingizie kitu chochote nje ya hapo. Na ndiyo maana ni hatari sana
kwa mzazi kumpeleka mtoto wake chini ya umri huu shule za boarding kwa sababu
huu ndiyo umri ambao mtoto anatakiwa apewe msingi bora wa maisha ikishindikana
hapo basi tena.
Kwa hiyo kitu cha msingi katika umri ni kumpa mtoto malezi bora
yatakamfanya ajitambue zaidi. Malezi haya kwa bahati mbaya tofauti na wengi
wanavyofikiri hawezi kupewa na mwalimu au na mtu mwingine yoyote kwa ubora wa
hali ya juu zaidi ya mzazi. Kwani ni kipindi ambacho unatakiwa umfundishe mtoto
wako juu ya mambo mengi kama upendo, kujali, utunzaji mzuri wa fedha, utu,
kuokoa muda, kutoa, kujiamini na mambo mengineyo mengi.
Kwa kukosa mambo hayo baadae hupelekea mtoto huyu kuanza kuteseka
kujifunza upya na tena kwa tabu lakini kumbe wakati alitakiwa kujifunza akiwa
mdogo tena kwa urahisi . kwa kulijua hili leo unaweza ukaanza na kumfundisha
mtoto wako namna ya kumjengea mtazamo chanya ambao utamfanya ajiamini na
kufanya vizuri katika kila eneo la maisha kwa ubora wa hali ya juu.
Je, unawezaje kumjengea moto wako mtazamo chanya?
1. Msifie.
Jijengee tabia ya kumsifia mtoto wako kwa yale mambo madogo
anayoyafanya. Acha kumkosoa na kiasi cha kwamba kujiona hafai. Hakikisha unampa
sifa. Sifa hizo itakuwa nzuri sana kama utakuwa unampa hadharani mbele ya
wenzake. Hilo litamfanya ajiamini zaidi na kujiona yeye anaweza. Kwa kadri
utakavyoendelea kumsifia atajikuta mtoto wako anazidi kuwa mwenye uwezo mzuri wa
kujiamini sana.
MSIFIE MTOTO WAKO ANAPOFANYA JAMBO ZURI |
|
2. Mwamini.
Mbali na kumpa sifa, lakini pia unaweza kumjengea mtoto wako tabia
nzuri ya kujiamini kwa wewe kumwamini pia katika yale mambo anayofanya. Kama ni
kazi umemwachia, mwache aifanye akiwa peke yake huku ukiwa unamfatilia sio sana
ili kuona anafanyaje. Kwa kitendo cha kumfanyia hivyo atajiona kuwa yeye kumbe
anaweza kufanya mambo makubwa na hivyo atajikuta akiwa anajiamini.
3. Mpe majina mazuri.
Weka utararibu wa kumpa mtoto wako majina mazuri yatakayomfanya
ajiamini. Kila unapokutana naye mbali na kumuita jina lake halisi unaweza
ukamuita ‘Pilot, shujaa, mshindi, mtaalamu’ na mengineyo mengi
yatakamfanya ajiamini na kujiona bora kuliko. Epuka kumpa ‘lebo’ za
kumuita majina kama vile ‘mjinga wewe, kichwa maji we’. Hiyo itamkatisha
tamaa na itamfanya ashindwe kujiamini.
4. Mpe mazoezi ya kuongea mbele za wenzake.
Anapokuwa na wenzake tafuta kitu cha kuongea na kumfanya aongee
mbele za wenzake. Hata kama anaona aibu mpe moyo wa kumfanya aendelee kuongea.
Kwa kitendo hicho kitamfanya azidi kujiamini sana na itampelekea kweli kuongeza
uwezo wake mkubwa wa kujiamini siku hadi siku. Hata wakati mwingine hata kuwa
na ule woga mkubwa ndani yake wa kuzungumza.
Unaweza ukafanya mambo mengi yatakayomfanya mtoto wako azidi
kujiamini. Lakini kwa leo fanyia kazi kwanza hayo na hakikisha mtoto wako
anaweza kujiamini kwa namna yoyote ile. Hiyo itamsaidia sana kwa maisha yake
yote ya baade.
Kwa makala nyingine nzuri pia tembelea DIRA YA MAFANIKIO kwa kujifunza na kuhamasika
kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,
No comments:
Post a Comment