Thursday 28 April 2016

UMUHIMU WA KUWA NA FAMILIA BORA ILI KUJENGA JAMII BORA.


Habari mpenzi msomaji wa wavuti hii? Na karibu katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza umuhimu wa kuwa na familia bora ili kujenga jamii bora. Bila familia bora hakuna jamii bora ambayo italeta maendeleo katika dunia. Tunapenda kujifunza mambo ya familia au tunasoma mambo ya familia kwa sababu kuu mbili;
Kwanza, sisi sote tumezaliwa katika familia. Hakuna mtu hapa duniani ambaye hajazaliwa katika familia ndio maana sisi sote tumezaliwa katika familia na tunapaswa kujifunza sana mambo ya familia.
Pili, familia ni msingi wa maisha ya mtu. Kila mtu anapata msingi wa maisha kutoka katika familia yake. Baba na mama wakimpatia mtoto msingi mzuri wa maisha yake basi mtoto atakwenda kujenga jamii iliyo bora kabisa. Ndio maana watu wako tofauti sana hii ni kutokana na kila mtu amepata msingi wa maisha tofauti na kuna wengine wamepata msingi mzuri wengine wamepata msingi mbaya.


Kwa kawaida familia inajengwa na baba, mama na watoto au mtoto. Familia ni kiungo cha msingi katika jamii. Mungu amepanga kila mtu kuzaliwa katika familia. Mtoto anajenga maadili na mtazamo wake kuhusu yeye mwenyewe, ulimwengu na maisha kutoka katika familia kulingana na mazingira alipozaliwa na alipokulia.
Ili tujenge jamii bora tunatakiwa kwanza tujenge familia bora kwa sababu kila mtu ametokea katika familia. Ndani ya familia baba na mama wanapaswa kuwafundisha watoto maadili mema tokea wakiwa wadogo kuwa mafunzo ya jinsi kuishi, kuwa na maadili mazuri. Mtoto akikosa kupewa upendo katika familia na kufundishwa falsafa hii kubwa ya upendo atakwenda kutengeneza jamii mbovu kama mtoto anatoka katika familia ambayo baba na mama wanaishi maisha ya uadui, ugomvi yaani kama vile maisha ya chui na swala. Mtoto anaona baba na mama wanapigana tokea akiwa mdogo je unafikiri anajenga nini katika akili yake? Baba ni mlevi wa kupindukia, wazazi wote wawili wanakosa upendo, hawaheshimiani wanatukanana mbele ya watoto, nyumba haina amani kila mtu na mambo yake matokeo yake wazazi wanapandikiza chuki kwa watoto matokeo yake ni kujenga jamii mbovu.
Familia ikiishi katika falsafa ya upendo tutajenga jamii bora yenye upendo. Upendo wa kujipenda wewe mwenye na watu mwingine. Familia ikikosa kuishi katika msingi imara wa upendo wanakwenda kujenga jamii ambayo haina hofu na mtu ambaye hana hofu atafanya kitu chochote anachojisikia na kuleta madhara makubwa kwa jamii. Kutokua na upendo hakuna huruma ya Mungu watu wanatenda mambo ya ajabu ambayo chanzo chake ni kukosa msingi bora kutoka katika familia.
Familia inayowajibika katika kufanya kazi kwa bidii, kila mmoja kutekeleza wajibu wake bila shuruti itajenga jamii bora. Familia kuwafundisha watoto kuwajibika ni mafanikio ya familia kuongeza kizazi kingine bora ambacho ndio jamii. Bila familia hakuna jamii. Jamii inapata faida kupitia familia, jamii inapata watu wanaowajibika kutoka katika familia. Familia ni mali ya jamii. Familia ikiwa nzuri na jamii itakua nzuri. Hivyo basi, familia ikiharibika na jamii inaharibika.
Watoto wanaathirika sana kisaikolojia wakiangalia matendo mabaya kutoka kwa wazazi. Mwisho wa siku watoto wanawachukia wazazi kwa matendo yao , watoto wanakata tamaa ya maisha na kuona hakuna sababu ya kuishi je kama familia imejengwa kwa msingi kama huu tutatengeneza jamii iliyo bora?

Mtu anafahamika katika jamii kama mtu wa familia fulani. Mtoto wa familia fulani na mzaliwa wa sehemu fulani. Kwa hiyo, familia inakuwa chanzo cha kujenga maisha ya mtu na familia ni muhimu sana katika malezi.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com

No comments:

Post a Comment