Tuesday, 13 May 2014

CHANGAMOTO ZINAZOSABABISHWA NA WANANDOA WENYEWE

Kama nilivyosema kwenye Utambulisho wa Blogu hii, kwamba makala yangu hii, itaongelea sababu za changamoto/migogoro inazosababishwa na wanandoa wenyewe.
Kabla sijaongelea changamoto zinazobabishwa na wanandoa wenyewe. Ni vizuri nikaongelea mahusiano yalipo kati ya ndoa na taifa yaani; mchango wa ndoa katika kujenga taifa na tabia za watu katika taifa lo lote. Ndoa ni chanzo cha taifa lo lote kuwa lilivyo hivi sasa yaani; kuwa na nguvu au dhaifu. Kama tujuavyo taifa hujengwa na hubolewa na watu wake, kwa sababu ndio wanaokuwa  viongozi, watunga sera, wakulima, wataalamu na wafanyakazi wakuu wa kila sekta wa taifa husika. Kama tujuavyo misingi ya tabia ya binadamu yo yote inaanza kujengwa/kubomolewa akiwa bado tumboni mwa mamaye na hatimaye akiwa mtoto mchanga chini ya baba na mama, mama pekee, baba pekee kutegemea na mazingira  Mungu aliyompanga mtoto huyu alilelewe. Mtoto hujengwa au hubomolewa vipi? Kimalezi akiwa tumbo ni somo refu sana, lakini kwa sababu si lengo la makala hii kufundisha somo hilo sitaliongelea. Mtoto akishazaliwa, walezi wake wakuu wanakuwa ni baba na mama, mama pekee, baba pekee, mtaa  pamoja na jamii inayomzunguka, huanza kufundisha mila na desturi za jamii husika. Ukilelewa katika familia ya wacha Mungu, wachapa kazi, wavuvi, waongo, watukanaji, wagovi na wewe utajifunza tabia hizo. Kimsingi kila binadamu huwa na mafungu mawili ya tabia yaani; tabia ya kujifunza na ya asili (kuzaliwa na nazo). Lakini hapo napenda kuongelea tabia zinazotokana na mazingira au za kufundishwa na zinaathiri vipi, maisha katika ndoa.
Kwa hiyo, mimi/wewe tabia nilivyo/ulivyo ni  matokeo ya malezi niliyopata/uliyoyapata katika makuzi yangu/yako nikiwa/ukiwa chini walezi wako pamoja na tabia ya asili yaani; yakuzaliwa nayo.
Ni vizuri pia, msomaji wangu ungefahamu kwamba familia huzaa jamii na jamii huzaa taifa.. Kwa tafsiri fupi isiyo rasmi; ndoa ni zao la familia, familia nyingi huitwa jamii na jamii nyingi ndio huunda taifa. Ndoa ni muunganiko wa hiari wa mtoto wa familia moja na nyingine wa jinsia tofauti kuwa mke na mme. Hapa neno mtoto limetumika kwa maana ya zao la familia si kwa maana ya umri. Ki-umri kila nchi ina sheria yake kuhusiana na umri unaofaa kwa msichana kuolewa. Kwa hiyo, ndoa ni muunganisha wa watu wawili waliolelewa katika malezi tofauti.
Changamoto za kwenye ndoa zinazosababishwa na wanandoa wenyewe chanzo chake kinaanzia kwenye malezi waliopata wanandoa husika katika makuzi yao. Malezi huzaa tabia na tabia kuna inayoletwa na mazingira na ya asili. Tabia ni somo kubwa ambalo linahitaji makala maalum.  Visababishi vya changamoto zinazotokana na wanandoa wenye ni matokeo ya tabia zao wenyewe wanandoa. Baadhi ya sababu hizo ni mawasiliano(kutoelewana), usaliti, udanganyifu, uchoyo, kukosa na maadili, n.k  na katika makala hii nitajadili changamoto ya mawasiliano.
MAWASILIANO (KUTOELEWANA)
Sababu hii ni chanzo kikubwa cha changamoto/migogoro mingi sana katika jamii nyingi sana katika dunia yetu hii.
Changamoto hii, kiini chake ni mmojawapo wa wanandoa au wote wawili kutotaka kumsikiliza mwenza mahitaji/mawazo yake iwe ya vitu au ya kimwili kwa ukaidi au kutokuwa na uwezo wa kutimiza au kutokuwa tayari kumsikiliza mwenza mantiki yake katika hitaji husika. Kwa lugha nyingine changamoto  hii ninaweza kusema ni kutoelewana.
Katika hali ya kawaida ukiona watu wawili ni marafiki sana ujue mmoja au wote wako tayari kusikiliza wazo la mwenzie kwa umakini na kulikubali au kulikata na kueleza sababu za kulikataa kwa kujenga hoja za kumshawishi sababu za kutokukubaliana nae pasipo kumuudhi mtoa wazo. Kusikiliza kwa makini nina maana huonyesha kihisia kwamba unajali hitaji lake. Kuonyesha kujali umfanya kujiona unanthamini kwa kiasi kikubwa na kumuondolea unyonge.
Hivyo hivyo pia,  katika ndoa ni muhimu sana kuheshimu hitaji la mwenzi wako na kulifanyia kazi. Kuliheshimu hitaji la mwenzi wako hakumaanisha kulikubali tu hata kama sio nzuri hapana, ila kama hukubaliani nalo toa sababu za msingi ni kwa nini hukubaliani na wazo husika na kutoa mawazo yako mbadala pasipo kuonyesha kupuuza/kudharau mawazo yake.
Kutimiziana mahitaji ya kimwili ni jambo moja la msingi katika ndoa. Lakini kikubwa hapa ni kwamba unalitimizaje? Ili, kuweza kuondoa malalamiko kwenye suala hili, kujuana ni jambo la muhimu sana. Na hili linawezeka kama wawili hawa  wakiwa  wazi katika hitaji hili. Hii inasaidia kujua namna ya kumuridhisha kila husika katika hitaji husika pasipo kumletea shida au kuleta malalamiko kutoka kwa mmojawapo wao. Ninaposema shida nina maana inatakiwa kila mmoja ajue njia muafaka ya kumridhisha  mwenzie. Kimsingi akina mama mara nyingi ni wa wanga wa kutoridhishwa na wenzi wao kwa sababu ya kutokuwa wa wazi au wenzie wao kuwa na ubinafsi zaidi kwa kutaka kuwatumia wenzi wao kama “Robot”. Robot ni chombo kinachotengenezwa na binadamu chenye uwezo wa kufanyishwa kazi kama binadamu kwa mfano; kufanyakazi viwandani, mashambani, kuongoza magari n.k.
Nisingependa kuwachosha kwa kuandika makala ndefu sana, visababishi vingine vya changamoto za ndoa vinavyosababishwa na wandoa wenyewe nitaendelea navyo kwenye makala itakayofuata.
Kwa ushauri kuhusiana na changamoto za ndoa na uchumba tuma jambo lo lote unalohitaji ushauri  kwenye anuani pepe fkmwamoto@gmail.com na utajibiwa kupitia anuani pepe yako.
Hili kuweza kuingia kwenye blogu yenye makala za ushauri mbalimbali wa migogoro ya mahusiano,  tuma shilingi elfu kumi tu (TZS. 10,000/=) kwenye airtel money 0784190882. Halafu nitumie anuani pepe yako na jina la usajili la laini uliyotumia kutuma pesa kwenye anuani pepe hapo juu. Hii ni ada ya kukuwezesha kuingia na  kusoma makala za Blogu hiyo, utapata maarifa/mbinu za kukabiliana changamoto za mahusiano, hivyo kujiepusha na magonjwa yaletwayo na changamoto hizo kama vile Shinikizo la damu, kisukari, UKIMWI n,k. Karibu TUJENGE TAIFA IMARA.

No comments:

Post a Comment